________________________
Na. Joseph Mayuni
Unapozungumzia historia adimu ya taifa langu Tanzania basi huwezi kuacha kutaja mkoa wa Tabora. Kwa maana ya kwamba, historia ya Tanzania haiwezi kukamilika kama hatujataja kabila la Wanyamwezi. Hapo nawataja washujaa kama Chifu Mirambo(Milambo) na Chifu Said Fundikila na wengine wengi ambao siwezi kuwataja kwa siku ya leo.
Kama hiyo haitoshi nawakumbusha tu kwamba ni Tabora ambapo uamuzi wa busara uliosimamiwa na chama cha TANU ambapo wazee wa Tabora wakisaidia na Mwalimu Julius Kambaraga Nyerere, ulifanyika Tabora mnamo miaka ya 1958. Basi wakati ukitafakari niliyokuambia hapo, yakupasa kutambua kuwa Tabora ilishajiwekea historia ya kuwa na sarafu yake. Hivyo kaa vizuri uweze kupata historia hii adimu.
Kwa majina naitwa Joseph Mayuni, kijana wa kiafrika ambaye napenda sana kufatilia mambo ya historia hasa inayohusu Afrika. Unaweza kusoma baadhi ya Makala zangu kupitia www.theafricanhistory.com ambazo kwa asilimia kubwa zimeandikwa kwa lugha ya kiingereza.
Na mara baada ya kukwambia hayo,ni kwmaba, mwaka huu nilipata nafasi ya kufika nchi ya Namibia kwa lengo la kujifunza mambo kadha wa kadha. Nilipata mwaliko kutoka kwa rafiki yangu ambaye napenda kumwita kwa jina la “Sara Diorf”. Katika kukutana naye nilibahatika kumkuta na kitabu ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kijerumani “Kaiserliches Deutschland” Kitabu kimeelezea mambo mengi sana yenye kuzungumzia Afrika. Na ndipo nilipopata kufahamu juu ya historia ya Sarafu ya Tabora, Wanyamwezi mpoooo……!!!!!
Ipo Hivi……..
Inapata kusimuliwa kuwa mara baada ya Ujerumani kupewa koloni la Tanganyika na sehemu zingine za Afrika mashariki mwishoni mwa miaka ya 1890. Japokuwa Wajerumani walikutana na changamoto kadha wa kadha, si unakumbuka habari za Mkwawa na Wajerumani miaka ya 1988? Mwisho wa siku Wajerumani walifanikiwa kutawala na kuanzisha baadhi ya mambo kwa manufaa yao. Waliweza kujenga ikulu zao huko Bagamoyo, Tanga na mwisho wa siku wakaja Tabora.
Ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 1905, Wajerumani walifanikiwa kuanzisha benki mjini Dar es Salaama iliyoitwa “Deutsch-Ostafrikanische” najua wengi hawajatamka hili neno. Na mnamo mwaka 1911 Wajerumani pia walianzisha benki nyingine huko mjini Tanga iliyopata kuitwa the Handelsbank fuer Ostafrika.
Malengo makuu ya kuanzisha banki hizo ni kukuza uchumi wa Ujerumani. Hivyo basi mwanzo mwa miaka ya 1912 Wajerumani walizidi kuwekeza kwenye koloni lao na kufanikiwa kufika tabora ambapo napo walitaka kuanzisha bank lakini ndio kilikuwa kipindi cha maandalizi ya vita ya kwanza ya dunia, hivyo mchakato huo ukafia njiani na badala yake walifanikiwa kuanzisha Sarafu ya Tabora ambayo ilianzishwa na kutumiwa miaka ya 1916.
Na lengo la kuanzisha sarafu ya Tabora ilikuwa ni kuongeza idadi ya sarafu ambazo zilikuwa zikitumika kama sehemu za mishahara kwa wanajeshi wa kijerumani na Waafrika ambao walipambana vita ya kwanza ya dunia kuanzia mwaka 1914-1918 upande wa wajerumani.
Sarafu ya Tabora Ilikuwaje?
______________________
Sarafu ya Tabora ilitengenezwa kwa madini ya dhahabu . Sarafu hii ilipata kubuniwa na bwana mmoja aliyefahamika kwa jina la Friedrich Schumacher. Sarafu hii ilikuwa na uzito wa gram 6.8.(6.8g)chini ya usimamizi wa bank ya Deutsch-Ostafrikanische. Sarafu hii ilikuwa na kipenyo cha milimita 22(22mm). Sarafu ya Tabora iliwakilisha mambo yafuatayo, Mlima wa Kilimanjaro ambao ni moja ya mlima mrefu hapa duniani ambapo kwa Afrika ni wa kwanza.
Hivyo ni sifa kwa Wajerumani kutawala sehemu ambayo ina mlima mrefu kuliko yote Afrika, Kilimo cha Katani ambacho ni moja ya kilimo ambacho kilianzishwa na mjerumani bwana Richard H mnamo miaka ya 1892.
Pia kwenye Sarafu ya Tabora kuna Herufi “T” ikiwa na maana ya Tabora kama sehemu ya biashara tangu miaka ya 1800. Kwa chini kuna mwaka umeandikwa 1916, ikiwa ndio mwaka ambao sarafu ya Tabora ilianza kutumika. Kuna tembo ikiwa ni mmoja ya mnyama ambaye amebeba utajiri mkubwa sana unaopatikana katika pembe zake. Kuna maneno yameandikwa Deutsch Asta Afrika ikiwa na maana ya Ujerumani ya Afrika Mashariki, sehemu ambayo Wajerumani wametawala.
Pia kwenye sarafu hiyo kuna neno “15 Rupee ikiwa na maana ya kwamba, sarafu moja ya Tabora ilikuwa na thamani ya Rupia 15. Na mwisho kabisa kwenye sarafu ya Tabora kunaonekana ndege aina ya Tai, ambapo kwa ujerumani huitwa Der Bundesadler yaanu “The Federal Eagle”. Tai ni moja ya ndege ambaye ana historia ndefu sana huko Ulaya tangu kipindi cha utawala wa Warumi.
Na ndege huyu ana mahusiano makubwa sana na mapambno kati ya makabila ya kijerumani yaliongozwa na Chifu Arminius dhidi ya utawala wa Kirumi wa Mfalme Julias Kaisari mwanzoni mwa miaka ya 10AD.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya sarafu za kale za kiafrika kama wakina Freeman Greenvile, Malvin Ember na bila kumsahau Dk.Kimiyoshi Matsumura, wanabainisha kuwa, sarafu ya Tabora ni moja ya sarafu bora na yenye kuvutia kwa wakati ule.
Ikumbukwe kuwa, mnamo mwaka 1914 -1916 dunia iliingia kwenye mapigano ya vita ya kwanza ya dunia. Ambapo kwenye vita hiyo Wajerumani walishiriki pakubwa sana. Na hivyo vita ya dunia kufika maeneo ya Tabora. Inasimuliwa kuwa WabelIgiji ndio walikuwa wa kwanza kuivamia Tabora wakitokea maeneo ya Kongo wakipitia Kigoma.
Na mwisho wa siku sarafu nyingi zilichukuliwa na washindi wa vita na zingine nyingi sana zilifukiwa katika maeneo kadha wa kadha katika ardhi ya Tabora na Singida. Wajerumani hawakutaka maadui zao wapate utajiri huo na ndio maana waliamua kuzificha sarafu hizo.
Habari za kufukiwa sarafu hizo zimejaa usiri sana kwani si rahisi sana mtu wa kawaida kujua zilipo maana kuna stori nyingi sana za mauzauza kuhusu sarafu za Tabora. Kwa masimulizi ya Wazee wa Tabora wanadai kuwa ufukiwaji wa sarafu za Tabora uliendana na masuala ya matambiko.
Lakini ikumbukwe kuwa, kutokana na sarafu hiyo kutumika kama sehemu ya mishahara kwa wapiganaji, kulikuwa na baadhi ya watu ambao walikuwa nazo mpaka sasa, lakini sehemu za makumbusho nchini Ujerumani kitengo cha Sarafu za kale unaweza kuzikuta sarafu za Tabora. Kwani moja ya ugunduzi mkubwa sana uliofanywa na wajerumani.
Yaliondikwa hap ani mkusanyiko wa maandiko na masimulizi ya wazee ambao nimekaa nao na kupata baadhi ya Habari ya Sarafu ya Tabora. Ni maandiko machache sana hivyo bado kunahitajika utafiti wa kina kuweza kupata kujua Zaidi kuhusu sarafu ya Tabora.